Ulinganishi Na Ulinganuzi Wa Tasfida Za Matibabu Katika Kiswahili Na Kimarachi
Patrick Oyinda, Ayub Mukhwana

Résumé
Kazi hii inahusu mikakati inayotumiwa kuibua tasfida za muktadha wa matibabu katika Kiswahili na Kimarachi kwa kujikita katika tasfida za tiba, ushauri nasaha, uhamasishaji na uasaji. Utafiti huu umechochewa na hali kuwa ulimwengu hivi leo unakumbwa na janga la ukimwi, magonjwa mengine hatari na vitendo fulani vinavyozua aibu na ambavyo huhitaji kuzungumziwa kwa lugha ya upole ili ujumbe uwafikie walengwa kwa njia isiyotisha, kukera au kuzua aibu. Hivyo basi, wazungumzaji wa Kiswahili na Kimarachi hawana budi kufahamu mikakati ya kuundia tasfida husika ili kudumisha upole katika lugha. Lengo la kazi hii ni kuangalia mikakati inayotumiwa kuibua tasfida za muktadha wa matibabu katika jamii lugha ya Kiswahili na Kimarachi. Kwa kutumia nadharia ya upole ya Brown na Levinson (1987) na nadharia ya ethnografia ya mawasiliano ya Dell Hymes (1974) katika uchanganuzi wa data, matokeo ya kazi hii yana umuhimu mkubwa sana kwa madaktari, wauguzi, wahamasishaji, waasaji, walimu, wanafunzi, wanasiasa na wazungumzaji wote kwa jumla wa lugha ya Kiswahili na Kimarachi. Tumetumia mbinu ya kusoma makala rasmi yaliyoandikwa katika Kiswahili sanifu ili kupata data ya Kiswahili. Data katika lugha ya Kimarachi tumeipata nyanjani kwa kutumia hojaji na vilevile mahojiano. Watafiti pia wametumia ujuzi wao kama wanafunzi wa Kiswahili na wazungumzaji wa Kimarachi kutathmini tasfida zilizopatikana. Imebainika wazi kuwa kuna mikakati mingi ambayo wazungumzaji wa Kiswahili na Kimarachi hutumia kuibua tasfida za kimatibabu. Hata hivyo, mikakati hii hutegemea swala la umri, uwili lugha, wingi lugha na kiwango cha elimu miongoni mwa wanajamii lugha husika.

Full Text: PDF     DOI: 10.15640/imjcr.v5n1a2